Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere akizungumza jambo.
WINGU LA HABARI
NA RACHEL MKUNDAI, TUNDUMA
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Charles Kichere ametishia kuwafutia leseni mawakala wa forodha wanaofanya
udanganyifu katika kadhia za wateja wao wanazoziwasilisha katika ofisi za TRA pindi
wanapotoa au kuingiza mizigo nchini kwani hizo ni njama za kuwepa kodi.
Bw. Kichere ametoa onyo hilo alipokuwa akizungumza
na mawakala wa forodha wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Tanzania na
Zambia uliopo katika mji mdogo wa Tunduma mkoani Songwe akiwa katika ziara yake
kutembelea mikoa ya nyanda za juu kusini.
Kamishna Kichere amesema kumekuwepo na baadhi ya
mawakala wa forodha ambao huwasilisha nyaraka zenye taarifa za uwongo au zinazoonesha
idadi pungufu ya bidhaa zilizopo kwenye mizigo tofauti na uhalisia.
“Kusema
ukweli sitawavumilia maajenti (mawakala) ambao watakuwa wanaongepea serikali,
nitafuta leseni zao, tukiwakamata mnaenda kubumba bumba nyaraka zenye ankara za
uwongo, nitafuta leseni” alisisitiza Kamishna mkuu wa TRA.
Hali kadhalika, Kichere amewataka mawakala wa
forodha hao kushirikiana na maafisa wa TRA kwa kutoa taarifa sahihi za kadhia
za wateja wao ili waweze kukadiriwa kodi stahiki wanayotakiwa kulipa na kuilipa
kodi hiyo kwa hiyari kwa kuwa wote ni watanzania wanaoshirikiana kujenga taifa
moja.
Nao mawakala wa forodha katika mpaka wa tunduma
wameufurahia ujio wa kamishna mkuu na kuahidi kushirikiana na maafisa wa TRA
kwa kuwa taasisi hiyo ni kiungo muhimu kati yao na wateja wao.
Mmoja wa mawakala hao Bw. Edwin Mwendo amesema ni
vyema mawakala wakatimiza wajibu wao kulingana na taratibu za forodha kwa
kuepuka rushwa na kuwasilisha kadhia zenye taarifa sahihi ili kuepuka mkono wa
sheria endapo watabainika kuwa wanakwepa kodi.
Mwakilishi mwingine wa wakala wa forodha Bw. Alan
Upamba amesema ili kuepuka migongano katika kazi za forodha ni vyema pande zote
mbili za maofisa wa TRA pamoja na mawakala kufuata taratibu zote za kiforodha
ambazo zitapelekea ukusanyaji mzuri wa kodi na hivyo kuleta maendeleo kwa
taifa.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndiyo yenye
mamlaka ya kuwasajili Mawakala wa forodha nchini na wanatakiwa kufanyakazi kwa
mujibu wa Sheria na taratibu za forodha na kuhakikisha kodi sahihi inalipwa kwa
Serikali bila kukwepa.
No comments:
Post a Comment