Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, kutoka kulia ni Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri Mamlaka ya Hali ya hewa (TMA) Samwel Mbuya pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa Dk. Hamza Kabelwa.
..........
WINGU
LA HABARI
NA NOEL
RUKANUGA
Serikali
na sekta binafsi zimetakiwa kuchukua tahadhari juu ya mvua kubwa zinazotarajiwa
kunyesha hivi karibuni katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Hayo
yamesemwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk.
Agens l. Kijazi wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu uchambuzi
wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika
kipindi cha mwezi machi na mei mwaka huu.
Dk.
Kijazi amesema kuwa katika kipindi cha mwezi machi na mei mwaka huu kutakuwa na
mvua za wastani katika maeneo mengi ya nchi, huku vipindi vya mvua chini wastani
zinatarajia kutokea katika maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Tanga.
“Vipindi
vya mvua kubwa vinatarajia katika msimu huu wa mvua za masika unatarajia
kuishia katika wiki tatu za mwezi mei mwaka huu” amesema Dk Kijazi.
Amesema
kuwa mvua hizo zinaweza kusababisha milipuko ya magonjwa, hivyo jamii na sekta
husika zinapaswa kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari za kiafya
zinazoweza kujitokeza.
Hata
hivyo Dk. Kijazi ameeleza kuwa mamlaka za maafa na wadau mbalimbali ni kipindi
cha kuchukua hatua stahiki ili kujiandaa, kupunguza na kukabiliana na athari
zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazotarajia.
Mwelekeo
wa msimu wa mvua kwa kipindi cha mwezi Machi na Mei mwaka huu.
Kutokana
na mifumo ya hali ya hewa iliyopo na inayotarajiwa kuwa na mvua za wastani
katika maeneo mengi ikiwemo ukanda wa ziwa Victoria pamoja na pwani ya kaskazini
ambapo kutakuwa na mvua za wastani hadi juu wastani.
Hata
hivyo katika maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Tanga yanatarajia kupata mvua
chini ya wastani, huku katika msimu wa mvua zilizoanza mwezi Novemba mwaka wa
jana (Mikoa ya Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mbeya, Iringa, Njembe
pamoja na Ruvuma) zinatarajia kuendelea kunyesha katika kiwango cha wastani
hadi juu ya wasatani.
Mvua
za Masika mwaka huu.
Msimu
wa mvua za masika kwa mwaka huu ni mahususi katika maeneo ya nyanda za juu Kaskazini,
Mashariki, Pwani ya kaskazini, Visiwa vya unguja na pemba, ukanda wa ziwa
Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa kigoma.
Katika
msimu wa masika mwezi machi hadi mei mwaka huu) mvua za wastani hadi juu ya
wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mashariki na magharibi mwa ziwa Victoria.
.........
MWELEKEO WA MVUA TANZANIA KIPINDI CHA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA MACHI - MEI 2018.
Angalizo:
.........
MWELEKEO WA MVUA TANZANIA KIPINDI CHA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA MACHI - MEI 2018.
Dondoo muhimu za msimu wa mvua za Masika kipindi cha
Machi-Mei 2018
Taarifa hii
inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu
wa mvua katika kipindi cha Machi - Mei 2018, ushauri na tahadhari kwa wadau
wa sekta mbali mbali wanaohitaji taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji
wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na
wanyamapori, maliasili na utalii, nishati na maji, mamlaka za miji, afya
pamoja na menejimenti za maafa. Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari zake
unaonesha kuwa:
a)
Mwelekeo wa msimu wa mvua kipindi cha Machi –Mei,
2018:
• Katika kipindi cha Machi hadi Mei,
2018 mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo,
vipindi vya mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi
ya maeneo yaliyoko Kaskazini mwa mkoa wa Tanga.
Kwa upande mwingine, mvua za msimu ambazo zilianza mwezi
Novemba, 2017 katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua (mikoa ya Dodoma,
Singida, Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na
Ruvuma) zinatarajiwa kuendelea kunyesha katika kiwango cha wastani hadi juu
ya wastani kama zilivyo tabiriwa
• Vipindi vifupi vya mvua kubwa
vinatarajiwa katika msimu huu wa mvua za masika na msimu wa mvua unatarajiwa kuisha katika
wiki ya tatu ya mwezi Mei, 2018.
b)
Athari
• Vipindi vifupi vya mvua kubwa
vinaweza kusababisha mafuriko na athari katika sekta mbalimbali.
c)
Ushauri
Sekta mbalimbali zinashauriwa kuchukua tahadhari na
kujiandaa ili kutumia vyema utabiri huu.
|
(I) MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA KWA
KIPINDI CHA MACHI -
MEI 2018
Kutokana
na mifumo ya hali ya hewa iliyopo na inayotarajiwa (kama ilivyoelezwa katika
kipengele Na. II cha taarifa hii), mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo
mengi. Hata hivyo, baadhi ya maeneo ya Ukanda wa ziwa Victoria pamoja na Pwani
ya Kaskazini yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Maeneo
machache ya kaskazini mwa mkoa wa Tanga yanatarajiwa kupata mvua za chini ya
wastani.
Kwa
upande mwingine, mvua za msimu ambazo zilianza mwezi Novemba, 2017 katika
maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua (mikoa ya Dodoma, Singida, Kigoma,
Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma) zinatarajiwa
kuendelea kunyesha katika kiwango cha wastani hadi juu ya wastani kama zilivyo
tabiriwa. Maelezo ya kina juu ya mwelekeo wa msimu wa mvua ni kama ifuatavyo:
1.
Mvua za Masika 2018 (kwa maeneo yanayopata
misimu miwili ya mvua)
Msimu wa mvua za Masika ni mahususi katika maeneo ya
Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki, pwani ya Kaskazini, visiwa vya Unguja na
Pemba, ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Katika
Msimu wa Masika (Machi hadi Mei 2018) mvua za wastani hadi juu ya wastani
zinatarajiwa katika maeneo ya mashariki na magharibi mwa Ziwa Viktoria, wakati
mvua za wastani kwa ujumla zinatarajiwa zaidi katika maeneo ya kusini mwa Ziwa
Victoria, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na Nyanda za juu kaskazini mashariki.
Maeneo ya mikoa ya Dar se Salaam, Pwani, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja
na visiwa vya Unguja na Pemba yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya
wastani, wakati mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya
kaskazini mwa mkoa wa Tanga.
1.1
Kanda ya Ziwa Viktoria: (Mikoa ya Kagera,
Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga):
Mvua
zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi machi, 2018 katika mkoa wa Mwanza
na kusambaa katika mikoa ya Geita, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga kati ya
wiki ya pili na ya tatu ya mwezi machi, 2018.
Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa
ya Kagera na Mara pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mikoa ya Geita, Mwanza na
Simiyu. Maeneo ya mkoa wa Shinyanga na maeneo yaliyo kusini mwa mikoa ya Geita,
Mwanza na Simiyu yanatarajiwa kupata mvua za wastani.
1.2
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa
ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini
mwa mkoa wa
Morogoro):
Mvua
katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi machi, 2018.
Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya
mkoa wa Dar es Salaam, mkoa wa Pwani, visiwa vya Unguja na Pemba, kaskazini mwa
mkoa wa Morogoro na kusini mwa mkoa wa Tanga. Maeneo yaliyosalia yaliyo
kaskazini mwa mkoa wa Tanga yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.
1.3
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa
ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua
katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Mwezi Machi, 2018 na
zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi
Mvua za Msimu (Novemba – Aprili) kwa maeneo
yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.
Mvua za msimu ambazo zilianza mwezi
Novemba, 2017 katika maeneo yanayaopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (mikoa ya
Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe,
Ruvuma, Lindi, Mtwara na maeneo yaliyo kusini mwa mkoa wa Morogoro)
zinatarajiwa kuendelea kunyesha katika kiwango cha wastani hadi juu ya wastani
kama zilivyo tabiriwa.
Izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua
kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za
wastani na chini ya wastani.
(II)
MIFUMO YA HALI
YA HEWA
Hali ya kupoa kwa Joto la
bahari katika eneo la ukanda wa tropikali ya Bahari ya Pasifiki inatarajiwa
kuendelea katika kipindi chote cha miezi ya Machi hadi Mei, 2018. Kwa upande
mwingine, hali ya joto la bahari la wastani inatarajiwa katika eneo la
magharibi mwa bahari ya Hindi.
Hata hivyo, kusini magharibi mwa bahari ya Hindi
kunatarajiwa kuwa na joto la juu ya wastani katika kipindi cha Machi hadi Mei,
2018. Joto hilo litaendelea kuongezeka katika kipindi cha msimu wa Masika 2018
na ongezeko hilo hususan katika eneo la kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi
linatarajiwa kusababisha matukio ya vimbunga katika bahari ya Hindi.
Aidha,
hali ya kuendelea kuwa na joto la chini ya wastani katika bahari ya Atlantiki
(pwani ya Angola) inatarajiwa kuongeza msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka
misitu ya Kongo hivyo kusababisha ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo
nchini.
(III)
ATHARI NA
USHAURI
Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori
Unyevunyevu wa kutosha
kwenye udongo unatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki
(mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), kanda ya ziwa (Mikoa ya Kagera,
Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu) na Pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar es
Salaam, Pwani, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba).
Wakulima katika maeneo
hayo wanashauriwa kuendelea na maandalizi na kufanya shughuli za kawaida za kilimo. Hata hivyo,
eneo la kaskazini mwa mkoa wa Tanga linatarajiwa kuwa na vipindi vya upungufu
wa unyevunyevu katika udongo hivyo wakulima wanashauriwa kupanda mazao
yanayostahimili mvua chache na kukomaa mapema.
Maji na malisho pamoja na
upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuongezeka katika kiwango cha
kutosheleza kutokana na mvua za wastani hadi juu ya wastani zinazotarajiwa.
Hata hivyo, kwa matumizi sahihi ya utabiri huu, wakulima, wavuvi na wafugaji
wanashauriwa kutafuta na kupata ushauri zaidi kutoka kwa maafisa ugani. Hatua
za kuvuna maji ya mvua zichukuliwe kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa maji
wakati wa kiangazi.
Nishati, Madini na Maji.
Ongezeko
la maji katika mabwawa linatarajiwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za
wastani hadi juu ya wastani. Aidha, Wakulima na Wafugaji wanashauriwa kuvuna
maji kwa ajili ya matumizi ya baadae. Wachimbaji madini katika migodi
midogomidogo wanashauriwa kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo
linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi.
Maeneo
yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani (kaskazini mwa mkoa
wa Tanga) kina cha maji katika mabwawa kinatarajiwa kupungua, hivyo matumizi
mazuri ya maji kwa ajili ya shughuli mbali mbali ikiwemo uzalishaji umeme
yazingatiwe. Ili kukabiliana na upungufu unaoweza kujitokeza katika uzalishaji
umeme kwa kutumia rasilimali maji inashauriwa kutumia nishati mbadala.
Mamlaka za Miji
Vipindi
vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika msimu wa mvua, hivyo mamlaka za miji
pamoja na wananchi wanashauriwa kuchukua hatua stahiki. Hatua hizo ni pamoja na
kuhakikisha kuwa mifumo na njia za kupitisha maji zinafanyakazi katika kiwango
cha kutosha ili kuepusha maji kutuama na kupelekea mafuriko na uharibifu wa
miundombinu pamoja na upotevu wa maisha na mali.
Sekta ya Afya
Mvua za wastani na juu ya
wastani zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo zinaweza kusabibisha milipuko ya
magonjwa hivyo ushauri unatolewa kwa jamii na sekta husika kuchukua hatua
stahiki ili kupunguza athari za kiafya zinazoweza kujitokeza.
Menejimenti ya Maafa
Mamlaka za maafa na wadau
wengine wanashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kujiandaa kupunguza na
kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazotarajiwa.
Vyombo vya habari
Vyombo vya habari
vinashauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali
ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kutumia wataalam wa
sekta husika katika kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya
hewa kwa jamii.
Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na
wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee
kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
Mwelekeo
wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na
hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa
mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika
uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
Watumiaji wa taarifa za utabiri
huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama
unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea
kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa
mvua nchini.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania:
No comments:
Post a Comment