Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa majisafi na majitaka jijini Dar es salaam.
WINGU LA HABARI
Kufuatia changamoto za huduma bora za Majisafi na Majitaka katika jiji la Dar es salaam Serikali imeamua kukutana na wadau mbalimbali ili kuweza kujadili namna ya kuzikabili changamoto hizo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema aliyezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Mjema amesema kuwa ili kuendana na malengo ya Serikali ya kuhakikisha kuwa asilimia 95 ya wananchi wanapata huduma ya maji ifikapo mwaka 2020 ni lazima kukaa na wadau mbalimbali kujadili na kufikia maazimio ambayo yatakuwa suluhu ya matatizo ya maji jijini humo.
Amesema kuwa maji yanayozalishwa hivi sasa ni mengi na yanakidhi zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji hivyo basi uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam amewahakikishia wananchi wa mkoa huo watapata huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2020 iwapo watakaa na wadau wote kuona namna bora ya ufanisi wa kuyasambaza maji yote yanayozalishwa hivi sasa.
"Leo tumekutana na baadhi tu ya wadau wetu wa Maendeleo ambao wamekuwa wanatusaidia sana katika suala zima la kuhakikisha tatizo la maji linapungua",alisema.
DC Mjema amewashukuru WaterAid kwa kuweza kufadhili kikao hicho ambapo amesema anatambua kuwa wadau wote walioshiriki wanatambua kuwa wananchi wa Dar es salaam wana kiu ya huduma bora ya maji.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maji DAWASCO Mhandisi Aron Joseph, amesema wamejipanga kuhakikisha wanafikia asilimia 95 ya usambazaji wa maji jijini humo ifikapo mwaka 2020 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa WaterAid Henry Horombe ambao ndio wadhamini wa mkutano huo amesema zaidi ya shilingi Bilioni 17 zinahitajika katika mkoa wa Dar es salaam ili kupunguza changamoto mbalimbali za majisafi.
"Tunajitahidi kuja na njia tofauti za kuweza kuwafanya wadau waweze kukutana na kujadili pamoja na kuweza kufikia malengo kwa muda mfupi zaidi,alisema.

No comments:
Post a Comment