Na, Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa wakadiriaji
majenzi Afrika unaotarajiwa kufanyika Agost18-19 mwaka huu jijini Dar es
salaam.
Hayo yamesemwa leo na Rais wa chama cha
wakadiriaji majenzi Tanzania (TIQS) Samuel Marwa ambapo amesema kuwa Tanzania
kwa mara ya kwanza imekuwa mwenyeji katika mkutano huo ukiwa na lengo la kukuza
fani ya ukadiriaji majenzi ili mchango wake katika jamii uweze kutambulika.
Amesema mada kuu ya mkutano huo ni kufikia
malengo ya maendeleo endelevu na mchango wa huduma za ukadiriaji majenzi hivyo
sekta ya ujenzi na hasa miundombinu ni moja ya vipaumbele vilivyoainishwa kama
kichocheo cha kuwezesha kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kukuza uchumi
wa nchi.
“Malengo ya Maendeleo Endelevu yanakusudia
kuondoa umaskini na kupambana na udhalimu na kuleta usawa pamoja na kukabiliana
na mabadiliko ya tabia ya nchi kufikia mwaka 2030, hivyo mada hii inaendana na
na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta maendeleo yenye usawa,
mafanikio na ustawi wa kila mwananchi”alifafanua Rais huyo.
Aidha, amesema kuwa huduma hizo, zikitumika kwa
ukamilifu zitasaidia kupambana na rushwa na uwajibikaji dhaifu kwani huduma
hiyo ni nguzo muhimu katika kuchangia ufanisi na udhibiti wa gharama za
ujenzi na ukamilishaji kwa muda wa miradi na kupata dhamani ya
fedha.
Mbali na hayo Rais huyo ameuomba uongozi wa
vyuo tofauti nchini kuanzisha na kuzidi kudahili wanafunzi katika taaluma ya
ukadiriaji majenzi ili kutatua changamoto zilizopo.
Nchi zaidi ya 16 za Afrika zilizoko Jumuiya ya
Madola ikiwemo Angola na
Msumbiji zinatarajiwa
kushiriki katika mkutano huo.

No comments:
Post a Comment