|
Na Kelvin
Lyamuya.
Utaona fulana
zenye picha ya mtu huyu zikichukua nafasi kubwa, Ndio. Utacheka kwa furaha
pale utakapoona picha mitandaoni pamoja na video mbalimbali zilizotengenezwa
kwa mfano wake.
Na najua katika akili yako ni nini unachofikiria kwa sasa,
maisha ya Liverpool chini ya Jürgen Klopp. Ndio kwanza akitimiza siku kadhaa
tangu atangazwe rasmi kama mrithi wa Rodgers, Jürgen Klopp ameleta taswira
mpya katika mioyo iliyojeruhiwa ya wana 'Kop' duniani kote, ilikuwa ni zaidi
ya Shayiri nzuri kwenye kilevi cha ndugu zangu wa kule Marangu.
Kama
wachezaji wa Liverpool wataelewa nini akitakacho Klopp na kwa muda gani, basi
amin nakwambia ile 'Golden sky' ambayo mashabiki 45,000 wanaiimba kila
wikiendi pale Anfield wataifikia tena,haiko mbali sana ni kiasi cha kusubiri.
Ingawa ameshaweka wazi kuwa mapambano ndio yanaanza sasa, Klopp, amewasili
katika kipindi kigumu, Liverpool tayari imeshacheza michezo nane ya Ligi Kuu
England, na asilimia 80 ya wachezaji wa kikosi cha kwanza wapo kwenye
majukumu ya Taifa mpaka katikati ya wiki hii, na kama hiyo haitoshi Nahodha
wa timu, Jordan Henderson naye ni majeruhi.
Hakuna mechi za kirafiki ambazo
zingemsaidia kupata aina na mfumo mzuri katika timu, dirisha la usajili nalo
limefungwa labda angepata wachezaji wa kuweka sawa kikosi. Miezi miwili na
nusu iliyobaki ni kuipa timu morali, kuwaelewa na kuwaweka pamoja, na wakati
huo huo azoee mji mpya, tamaduni pamoja na Ligi kwa ujumla. Ni kazi ngumu kwa
yeyote yule, hata kwa mtu wa kariba na kujiamini kama Klopp. Labda alikuwa
sahihi kusema Liverpool ipo katika njia sahihi kwa kiasi fulani, lakini kuna
sehemu mbalimbali zenye kasoro katika klabu zinatakiwa kurekebishwa na muda
ndio hivyo tena hautoshi kufanya yote hayo, huku kwetu wanategemea makubwa na
inabidi wawe hivyo hivyo, Imani. Klopp amewasili katika kipindi ambacho
mashabiki wa Liverpool wana manung'uniko kuona heshima ya klabu yao imeshuka,
imekuwa kama kiroba cha kilo 20, Liverpool imekuwa nyepesi sana hivi karibuni
na huo ndio ukweli wenyewe. Sina shaka naye, ameonyesha wazi jinsi gani
heshima inavyotafutwa kwa njia yoyote ile, enzi za Signal Iduna Park.
Ni muda
wa kupambana kwa uhodari, kujitoa, na kufanya kazi kwa umoja, nikimaanisha
'Utatu Mtakatifu' wa mashabiki, wachezaji na kocha kuungana katika njia moja.
Mafanikio. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, mara kwa mara kulikuwa
na kasoro katika sera ndani ya klabu pamoja na kutosikilizwa kwa mawazo ya
wale wanaoamini kitu flani hakiendi sawa kwa hiyo kifanywe hiki, ilichangia
katika kufifisha vitu viwili ambavyo ni MUHIMU katika klabu- matokeo ya
uwanjani na furaha ya mashabiki.
Soka imekuwa ni mchezo mgumu pengine kuliko
kipindi cha nyuma, lakini bado yale mambo ya msingi yanatakiwa kufuatwa;
klabu yoyote yenye mafanikio ni ile ambayo mawazo, malengo yameungana kwa
pamoja hivyo kufanya kazi inakuwa ni rahisi, hakuna mizozano.
Mashabiki wa
Liverpool wamemuamini Klopp kwa asilimia zote, na wamempa muda wa kuwasilisha
falsafa zake ndani ya Anfield. Tunaishi katika umri wa kutegemea makubwa bila
kufikiri ni njia gani hasa ya kuyapata. Kwa ujio wa Klopp makubwa yanaweza
kutokea. Pia atawafanya wachezaji wa Liverpool kuitumikia klabu kwa moyo
wote, wakiwa chini ya kocha mwenye hadhi kama yeye hilo halina maswali. Kama
kutakuwa na manung'uniko, uchovu kwa kipindi alichokuwepo Rodgers, basi
katika kipindi cha wiki moja tu kila kitu kitakuwa sawa. Atawahitaji
wachezaji kwa asilimia zote, ndio, watafanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya
kuleta kile wasemacho "Total Footbal", aina ya soka analolihusudu
sana kocha huyu. Timu zinachocheza soka la kuvutia, zile zilizofanikiwa,
hazitegemei bahati ila ni kuchapa kazi ndio silaha yao.
Kama wachezaji wa
Liverpool wanahitaji hisani, wanatakiwa kufanya kile Klopp anachokitaka,
mchana na usiku. Kama wana wasiwasi kwamba ni kitu gani watakachokipata kama
wakifanya kazi kwa umoja na bila kuchoka basi warudishe kumbukumbu nyuma,
enzi Klopp anafundisha timu za Mainz 05 na Borussia Dortmund, kule anatajwa
kama gwiji wa kuheshimika. Klopp wakati anahojiwa siku ya Ijumaa, kuna neno
moja alisema ukilitathmini kwa umakini utaelewa, “Kuingia katika klabu sio
jambo la muhimu sana kuwafanya watu wakufikirie, wafanye watu wakukumbuke
pale unapoondoka." Wajerumani kadhaa walipita Anfield, wakafanikiwa,
basi kama Klopp ni kama waliopita, Kops mpo katika njia moja ya mafanikio,Willkomen Jürgen Klopp.
|
|
|
Post Top Ad
Responsive Ads Here
Thursday, October 15, 2015
Home
Unlabelled
WILLKOMEN JÜRGEN KLOPP KARIBU JÜRGEN KLOPP "THE NORMAL ONE"
WILLKOMEN JÜRGEN KLOPP KARIBU JÜRGEN KLOPP "THE NORMAL ONE"
About Unknown
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Responsive Ads Here
No comments:
Post a Comment