Taasisi inayojiusisha na maswala ya twakimu na utafiti TWAWEZA jana imetoa taarifa juu ya mambo mbalimbali waliofanyia utafiti ikiwemo Afya, uchumi,pamoja maswala ya kisiasa katika mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 25 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya utafiti huo mbele ya waandishi wa habari Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema kuwa matokeo hayo ni ya utafiti wa
hivi karibuni uliofanywa na taasisi hiyo kwa kukusanya taarifa za madodoso
kutoka kwa washiriki utafiti zaidi ya 1,300 wa Tanzania Bara.
Katika
matokeo hayo ya utafiti ulionesha kuwa iwapo uchaguzi ungefanywa leo, Mgombea
urais wa CCM, Dk Magufuli angeibuka mshindi huku akimshinda mpinzani wake wa
karibu, Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa
ambaye ana asilimia 25.
Eyakuze alisema wahojiwa hao walipoulizwa wanajisikia kuwa karibu zaidi
na chama gani, asilimia 62 walisema wako karibu na CCM huku Chadema ikipata
asilimia 25 na vyama vingine vikiambulia asilimia moja.
“Utafiti
wetu tunaomba ueleweke, tuliwauliza wananchi maswali bila kutaja majina ya
wagombea na wao katika swali la unadhani uchaguzi ungefanyika leo, ungemchagua
nani, asilimia 65 walisema watamchagua Magufuli na asilimia 25, walisema Lowassa,”
alifafanua Eyakuze ambaye alibainisha kuwa utafiti ulifanyika katika mikoa yote
ya Tanzania Bara.
Katika
utafiti huo uliofanywa mapema Agosti hadi Septemba mwanzoni mwaka huu, wahojiwa
waliulizwa swali ni mgombea yupi watampigia kura na kwa nini, na majibu
yalikuwa asilimia 26 walisema watampigia Magufuli kwa sababu ni mchapakazi huku
asilimia 12, wakisema watampigia Lowassa kwa sababu ya kutaka mabadiliko.
Aidha,
mkurugenzi huyo wa Twaweza alisema vigezo muhimu vinavyohusu makundi mbalimbali
ya watu vilitumika kuchambua ni nani au makundi gani yanayowaunga mkono mgombea
wa CCM, Dk Magufuli na Lowassa.
Hata
hivyo, makundi ya vijana na wasomi zaidi na wakazi wa mijini walionekana zaidi
kumuunga mkono Lowassa, huku makundi ya watu wazima na wenye elimu ya kiasi na
wakazi wa vijijini wakimuunga mkono Dk Magufuli.
Hata
hivyo, katika makundi hayo yote bado Dk Magufuli ameonekana kuongoza; mfano,
asilimia 57 ya watu wenye umri wa miaka 18 – 29 na asilimia 76 ya watu wenye
umri wa 30 – 39 wanamuunga mkono.
Huku
asilimia 33 ya wananchi wenye umri wa miaka 18 – 29 na asilimia 30 ya wenye
umri wa miaka 30 – 39 wanamuunga mkono Lowassa, tofauti na asilimia 15 ya watu
wenye umri zaidi ya miaka 50.
Hata
hivyo, utafiti huo ulibainisha kwamba kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka
2012 hadi sasa, bado wananchi wana imani na CCM kwa asilimia kubwa
ukilinganisha na vyama vingine.
Mchanganuo
wa imani hiyo kwa wananchi kwenye nafasi ya udiwani hadi urais, wananchi wengi
wameonesha bado wana mapenzi na CCM ingawa kuna kupungua kwa asilimia, ila bado
vyama vingine havikuweza kukishinda.
Nafasi
ya Urais mwaka 2015, CCM, imeonekana kuongoza kwa 66%, Chadema 22%, CUF 1% na
nafasi za ubunge CCM imeonekana kuongoza kwa asilimia 60, Chadema 26%, CUF 3%,
NCCR-Mageuzi na ACT- Wazalendo 1%.
Aidha,
utafiti umebaini kuwa CCM inaungwa mkono kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na
kwamba Chadema ni chama cha pili kinachopendwa kushinda vyama vingine vya
upinzani, ingawa wananchi wengi hawakukiunga mkono chama hicho kwenye nafasi
mbalimbali za wagombea.
Akizungumzia kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Eyakuze alisema
katika utafiti huo yapo maswali yaliyouliza iwapo wananchi wanaelewa maana ya
Ukawa ni nini.
Katika
majibu yao, utafiti huo ulibainisha kuwa asilimia 43 ya waliohojiwa walisema
wanafahamu kwamba Ukawa ni chama cha siasa kilichosajiliwa Tanzania na asilimia
33, walisema hawafahamu kama ni chama cha siasa.
Aidha,
asilimia 57 ya waliohojiwa walisema katika Uchaguzi Mkuu ujao, Ukawa itaonekana
kwenye karatasi ya kupigia kura. “Hapa ndio kuna kazi ya kuelimisha wananchi
kuwa Ukawa sio chama cha siasa na hakitakuwepo kwenye makaratasi ya kupigia
kura,” alisisitiza Eyakuze.
Maoni
kuhusu utafiti Baadhi ya wanachama wa vyama vya siasa na wanaharakati wamesema
matokeo ya utafiti ni maoni na yanaweza kubadilika wakati wowote. Wamesema
uchaguzi huu ni tofauti ukiwa mgumu na kuwa na mtikisiko wa kisiasa wenye
ushindani ulio mkubwa.
Akitoa
maoni yake baada ya kuzinduliwa kwa utafiti huo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema nusu ya wapiga kura
wanaamini kuwa Ukawa ni chama cha siasa jambo ambalo sio sahihi huku vyama vya
siasa vikitakiwa kutoa elimu zaidi kwa umma.
“Mseto
wa vyama vya upinzani, Ukawa unajumuisha vyama vinne vya siasa ambapo uliundwa
ili kuwawezesha wanachama kuingia katika uchaguzi huu wakiwa na Ilani moja na
mgombea mmoja kutoka chama kimojawapo kwa kila jimbo,” alisema Dk Mkumbo ambaye
pia ni mwanachama wa chama cha ACT - Wazalendo.
Alisema
mseto huo haujasajiliwa kama chama cha siasa na jina la Ukawa halitokuwepo
katika karatasi za kupigia kura na kuvitaka vyama kutoa elimu kuhusu hilo.
Aidha, alisema utafiti huo ni maoni tu kutoka kwa wananchi sio matokeo halisi
ya uchaguzi na kwamba tafiti za aina hiyo zipo duniani kote.
“Kwa
mfano nchini Kenya, wakati wa uchaguzi ambapo moja ya utafiti uliofanyika humo
kwa siku moja ulimtangaza Odinga (Raila) kuongoza na kesho yake kubadilika
ukimtangaza Kenyatta (Uhuru) kuongoza,” alisema Mkumbo.
Aidha,
alisema utafiti wa Twaweza ni wa 27 ambapo wamekuwa wakitoa tafiti
zinazoheshimika na kwamba ni muhimu kujenga tabia ya kupinga tafiti kwa utafiti
mwingine. Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa chama cha
NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura alidai matokeo ya utafiti huo yamepikwa na CCM
kupitia kwa mawakala wao wanaofanya kazi katika taasisi hiyo ili kuhalalisha
utafiti uliofanywa na chama hicho.
Mratibu
wa Kitaifa wa Mtandao wa Asasi zisizo za Kiserikali za Haki za Binadamu Kusini
mwa Afrika (SAHRINGON), Martina Kabisama alisema endapo Watanzania wangehojiwa
leo, wangeweza kutoa majibu tofauti na yaliyotolewa na Twaweza kwa kuwa mwamko
ni mkubwa zaidi wa kisiasa kadri siku zinavyosonga mbele.
No comments:
Post a Comment