WINGU LA HABARI
Mapato yanayotokana na mauzo ya korosho katika
msimu wa 2017/2018 katika mikoa minne ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma,
yamepanda na kufi kia Sh trilioni 1.08 ikilinganishwa na misimu miwili
iliyopita.
Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho
Tanzania (CBT), Hassan Jarufu, wakati akifafanua juu ya uzalishaji na mauzo ya
zao la korosho nchini hadi kufikia mwisho wa mwaka 2017.
Korosho ni zao la biashara linaloongozwa kwa Tanzania. Inaiingizia
Tanzania takribani asilimia 15 za fedha za kigeni. Kwa mujibu wa Shirika la
Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), kwa Afrika, Tanzania inashika
nafasi ya nne kwa uzalishaji wa korosho ikizalisha asilimia 20 ya korosho zote,
lakini kwa duniani, inashika nafasi ya nane.
Kwa Afrika inazidiwa na Nigeria, Ivory Coast na Guinea- Bissau. Zao
la korosho linalimwa na kustawi zaidi katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na
Ruvuma. Jarufu, katika taarifa yake juzi alisema; “Ukiangalia msimu wa mwaka
2015/2016, utaona kuwa korosho zilizozalishwa zilikuwa kidogo zaidi.
Msimu huo ziliuzwa kilo 155,244,645 zikiwa na thamani ya shilingi
388,474,530,906 ikilinganisha na msimu wa 2016/2017 ambapo jumla ya kilo
265,237,845 ziliuzwa zikiwa na thamani ya shilingi 871,462,989,284,” alisema.
Alisema katika minada 10 ya msimu wa 2017/2018, mauzo ya korosho
yamefikia kilo 285,828,205 zenye thamani ya Sh 1,082,200,383,581. “Mnada wa 10
ulikuwa Desemba 21, 2017 na minada bado inaendelea kwa msimu wa 2017/2018,”
alisema.
Akidadanua mauzo hayo kwa kila mikoa hadi kufikia mnada wa 10,
Jarufu alisema Mtwara umeongoza kwa kuuza tani 178,165.741 zenye thamani ya Sh
701,674,466,366 ukifuatiwa na mkoa wa Lindi ambao umeuza tani 68,687.504 zenye
thamani ya Sh 247,163,294,296.
“Mkoa wa Ruvuma umeuza tani 19,545.613 zenye thamani ya shilingi
76,173,400,063 na mkoa wa Pwani umeuza tani 19,429.347 zenye thamani ya
shilingi 57,189,224,856 na kufanya mapato yote kwa mwaka huu kufikia shilingi
trilioni 1.082,” alisema.
Jarufu alitoa ufafanuzi huo baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 kwa
msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi.
Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “Korosho ni dhahabu ya kijani,
tuitunze, itutunze”. Alimweleza Waziri Mkuu kuwa, Bodi ya Korosho Tanzania kwa
kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele iliyopo Mtwara,
Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za wilaya, imeendelea kutekeleza mpango wa
miaka mitatu wa kupanda mikorosho 10,000,000 kila mwaka.
“Katika mpango huu, wastani wa mikorosho 5,000 inatarajiwa kupandwa
katika kila kijiji au mikorosho 30 kwa kaya kwa mwaka, sawa na ekari 330,000
kwa mwaka kwa nchi mzima.
Lengo la mpango huu ni kuongeza kiasi cha korosho kinachozalishwa
nchini kwa kuongeza wigo wa halmashauri zinazozalisha korosho na kupanda miche
inayotokana na mbegu bora zenye uzalishaji mkubwa na zenye ukinzani dhidi ya
magonjwa na wadudu,” alisema.
Alisema katika msimu wa 2017/2018, Bodi ya korosho inaratibu
uzalishaji wa jumla ya miche 14,001,820 ambayo imetokana na tani 100 (kilo
100,000) zilizozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele. Chanzo
habari leo.
No comments:
Post a Comment