WINGU LA HABARI
NA SALYM BITCHUKA, DAR ES SALAAM.
Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam pamoja na kuwawezesha wawekezaji wakubwa wa viwanda kufikia malengo yao na kuwajengea mazingira bora ya uwekezaji imepanga kujenga viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya wanawake,vijana na walemavu.
Hayo yamebainishwa leo na afisa maendeleo ya jamii mkuu wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam MARGARETH MAZWILE ambapo amesema Halmashauri ya jiji inaona kuna kila sababu ya kuendelea kuwasaidia wanawake,vijana na walemavu wanaopata mikopo kutoka halmashauri ya jiji kuwa mazingira wanayofanya shughuli zao sio rafiki na wanahangaika sana kutafuta masoko.
MAZWILE amesema mipango ya Halmashauri ya jiji ni kuendelea kujenga viwanda hivyo katika maeneo mbali mbali jiji ambayo itasaidia serikali katika juhudi zake za kufikia uchumi wa kati.
Aidha afisa huyo ametanabaisha kuwa katika bajeti ya mwaka huu wanatarajia kujenga viwanda kumi na mbili huku halmashauri ikitenga shilingi milioni mia sita kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo na tayari halmashauri imesha jenga viwanda vya shilingi milioni mia mbili hamsini ambavyo ni viwanda sita vya mwanzo.
Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam inawasaidia wajasiriamali hao kujitangaza zaidi ili waweze kupata masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi vile vile wataweza kubadilishana ujuzi na wenzao wa maeneo mengine, kufundishana wenyewe kwa wenyewe, kusaidiana na kupeana maarifa ya kutengeneza na kuuza bidhaa zao pamoja na ziara za mafunzo kulingana na uhitaji
No comments:
Post a Comment