Kuelekea siku ya haki za binadamu duniani inayoadhimishwa Novemba 10 kila mwaka, wadau wa kutetea haki za binadamu nchini wameitaka jamii pamoja na serikali kuhakikisha inakomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ambavyo sio rafiki kwa taifa.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya siku ya haki za binadamu iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC), leo Novemba 8 mwaka huu, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Tom Nyanduga amesema tume hiyo inakemea matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyotokea na kuitaka serikali kukomesha matukio hayo ili nchi isionekane kuwa haiheshimu haki za binadamu.
“Naungana na LHRC kuekemea yanayotokea na kuieleza serikali pamoja na wananchi kuhakikisha matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanakomeshwa, ili nchi isionekane kama haiheshimu haki za binadamu. Hizi ni dalili zinazotupeleka tusikotarajia, haya mambo hatukutegemea kutokea,” amesema Nyanduga.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Aidha, Bahame amevitaka vyombo vya dola kufanyia uchunguzi wa haraka kuhusu matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyotokea, pamoja na mahakama kutenda haki dhidi ya wahusika wa matukio hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba amesema serikali inabidi ichukue hatua katika kukomesha matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu ili kulinda haki hizo sambamba na kuifikia jamii yenye haki na usawa.
Wanakwaya wakiimba nyimbo ya yenye maudhui ya kupinga na kutetea haki za binadamu.
“Hivi karibuni Kumekuwa na ongezeko la matukio ya mauaji na utekaji nyara, kukamatwa kwa viongozi wa serikali hasa wa upinzani na kunyimwa dhamana, matukio ya kudidimiza uhuru wa habari, kuongezeka kwa matamko ya viongozi yanayo kinzana na haki za binadamu na matukio mengine. LHRC inaitaka Serikali kufanyia kazi mambo haya kwa ajili ya ulinzi wa haki za binadamu,” amesema.
Balozi wa Swedeni Tanzania, Mama Katarina Rangnitt ameitaka jamii kuendeleza mapambano katika harakati za kutokomeza ukiukwaji wa haki za binadamu, huku akizisisitiza taasisi zinazotetea haki za binadamu kuanzisha midahalo ya wazi yenye lengo la kuibua matukio hayo pamoja na kutoa elimu kwa jamii.
“Midahalo ya umma ni muhimu ili wananchi waelewe haki zao. Hakuna mtu aliye juu ya sheria, kila mtu inabidi afuate sheria. Tuendelee na mapambo ya kutetea haki za binadamu husasani kwenye kipindi hiki ambacho matukio haya yamekua yakitokea, tunahitaji wanaharakati wa haki za binadamu,” amesema.
Mwakilishi wa Taasisi za Kidini, Mkuu wa Idara ya Haki, Amani na Uadilifu wa Uumbaji katika Baraza la Maaskofu Nchini, Dkt. Camilius Kassala amesema “Asitokee mtu yeyote awachezee katika uhuru wa kuchagua, dhamira ya mema na mabaya na akili ya kujijua kama binadamu wenye haki ya kuthaminiwa.”
Amesema kuwa mambo yote mabaya yanayofanywa na baadhi ya watu yanakwenda kinyume na maandiko ya mungu katika biblia, hivyo ni vema yakafanyika mambo rafiki kwa taifa.
No comments:
Post a Comment