Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga (katikati) akionesha picha za viongozi na wanachama wa vyama vya siasa waliojerhiwa wakati wa uchaguzi wa marudio uliofanyika novemba 26/2017, kushoto ni Mwanasheria wa kituo hicho Willium Kahale na Ofisa Mwangalizi wa haki za binadamu, Alphonce Lusako
Na Noel Rukanuga
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani uvunjifu wa haki za binadamu na utaratibu wa usimamizi wa uchaguzi mdogo wa marudio wa udiwani uliofanyika Novemba 26/2017
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga amesema kuwa ni vema serikali kuendelea na mchakato wa katiba mpya kutoakan kuwapo kwa mahitaji ya tume huru ya uchaguzi pamoja na vyombo vya dola.
Wakili Henga amesema kuwa tathimini waliofanya wameweza kubaini ukiukwaji wa haki za binadamu katika uchaguzi huo uliofanyika novemba 26 mwaka huu.
"Kumekuwa na vitendo vya matumizi mabaya ya nguvu ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kukamatwa na kujeruhiwa lengo kuharibu na kuvuruga uchaguzi na kuwatia hofu wapiga kura, "amesema Henga.
Amesema vitendo hivyo vimeripotiwa kufanywa na vyombo vya dola ,watu wasiojulikana na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa vyama vya siasa ikiwemo Chama tawala(CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na vyama vingine vya upinzani.
Amefafanua kuwa Kata ya Kitwiru mkoani Iringa kulikuwa na utekwaji wa watu na wanaodaiwa kuwa ni vijana wa kikosi cha ulinizi cha CCM(Green Guard) kwa kuvamia na kuwateka wanachama wanaosemekana ni wa Chadema.
"Kushambuliwa gari la Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa Daddy Igogo na jeshi la polisi likimkamata na kumshikilia Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe... Lakini wapo mawakala walipigwa na walijeruhiwa wa wanachama wa vyama vya siasa, "amesema.
Amesema katika Kata ya Makiba, wakala wa Chadema Rashid Jumanne na mwenyekiti wa chama hicho tawi la Valeska, Nickson Mbise walijeruhiwa baada ya kushambuliwa kwa mapanga walipokuwa wakielekea katika vituo vya kupiga kura.
"Katibu wa CCM, wilaya ya Itimila mkoani Simiyu amelazwa hospitalini baada ya kushambuliwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema wakati akiwasindikiza mawakala wa chama kwenda kituoni kwa ajili ya kusimamia kura, "amesema.
Amesema vitendo hivyo katika Kata za Nyabubhinza, Maswa na Simiyu ambapo mawakala katika vituo 8 Kati ya vituo 13 walikamatwa na jeshi la polisi akiwemo Diwani wa Chadema Zakayo Wangwe.
Amesema kituo hicho kinaona matendo hayo si mazuri na yanaviashiria vya kukandamiza demokrasia hapa nchini.
"Kuna hatari ya kukuza utamaduni wa kulipiza visasi kwa chuki za kisiasa jambo ambalo litasababisha uvunjifu wa amani,"amesema.
Ametoa wito kwa serikali pamoja na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika kuhusika katika uvunjifu wa haki za binadamu na uvurugaji uchaguzi.
"Kituo kinatahadharisha kwamba matukio haya yasipokemewa na jamii nzima ni kiashiria kibaya na msingi mbaya utakaoathiri chaguzi zijazo ikiwepo uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi Mkuu 2020.
"Hii itasababisha kutishwa kwa wapiga kura wasijitokeze kutekeleza haki zao za msingi za kuchagua viongozi wao, kuchochea uhasama miongoni mwa wananchi na wadau wengine wa uchaguzi na kufifisha imani ya wananchi juu ya vyombo vya usimamizi wa uchaguzi na dola.
Mwanasheria wa Kituo hicho, Willium Hahale amesema kuna viashiria vibaya vya uvunjifu wa haki za binadamu katika chaguzi zijazo hivyo vyombo vya dola vinapaswa kufanya maandalizi ya kimfumo, sera na katiba ili kudhibiti vurugu wakati wa chaguzi zijazo.
"Vyombo vya dola vina jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafanyika vizuri si kuvuruga au kuwa chanzo cha vurugu, "amesema.
No comments:
Post a Comment