TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeteua Wabunge
wanane wa viti maalum wa Chama Cha Wananchi (CUF), baada ya waliokuwa wabunge
kwenye nafasi hizo, kufukuzwa uanachama wa chama hicho na Spika kuridhia.
Julai 24, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Prof
Ibrahim Lipumba alitangaza kuwafukuza ubunge wabunge hao wanane kwa makosa
mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu na kukihujumu chama huku moja ya mambo
yaliyotajwa ni ile ya kumuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif
Shariff Hamad (pichani) kwa kumuunga mkono kupambana na uongozi kwa kumsaidia
kufungulia ofisi maeneo ya Magomeni jijini Dar es Salaam kinyume na utaratibu.
Pia alitaja kuwa sababu nyingine ni ya
kukihujumu chama hicho, kwa maelezo kuwa walitaka kushirikiana na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumwondoa yeye (Lipumba) madarakani.
Juzi, Ofisi ya Spika wa bunge, ilitoa taarifa
kwa vyombo vya habari ikisema imepokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Taifa ya
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ikimuarifu kuhusu uamuzi wa Baraza Kuu la Chama
hicho kuwafukuza wabunge wanane na madiwani wawili uanachama wa chama hicho kwa
makosa kadhaa ya kinidhamu.
Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es
Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Kailima Ramadhani alisema jana
(juzi ) usiku walipokea barua kutoka kwa Spika, kuwataarifu uwepo na nafasi za
wabunge hao .
“Jana (juzi), usiku tulipokea barua kutoka kwa
Spika ikitutaarifu uwepo wa nafasi hizo na kututaka kutekeleza kwa kujaza
nafasi hizo, na sisi tuliwaandikia chama husika asubuhi na wakajibu na sisi
tukateua na kuwasilisha kwa Spika majina,” alisema Ramadhan.
Aliwataja wateule hao kuwa ni Rukia Ahmed
Kassim, Shamsha Aziz Mtamba, Kiza Hussein Mayeye, Zainabu Mndolwa Amir, Hindu
Hamis Mwenda, Sonia Jumaa Magogo, Alfredina Apolinary Kahigi na Nuru Awadh
Bafadhili.
Alisema majina yao tayari yameshawasilishwa kwa
Spika, kwa hatua nyingine na pia chama kimeshapewa nakala ya uteuzi huo.
Kailima alifafanua kuwa uteuzi huo ni kwa mujibu wa Ibara ya 78 kifungu kidogo
cha nne cha Katiba pamoja na kifungu kidogo cha 86, A(8) cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi Sura Namba 343.
“Tulipopata barua ya Spika, tulifanya kikao na
wajumbe wa tume leo (jana) na tuliwateua wabunge hao baada ya kuwasiliana pia
na chama husika na tayari tumeshapeleka majina kwa Spika,” alisema Kailima.
Aliongeza kuwa utekelezaji huo, umefanywa pia
kwa mujibu wa Kifungu namba 37 kifungo kidogo cha (3) cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi. Kwa upande wake, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Jafar Mneke
alisema wameshapata nakala ya majina ya wateule hao kutoka NEC.
“Baada ya Bunge kuridhia uamuzi wa chama wa
kuwafukuza wabunge wa viti maalumu wanane na madiwani wawili, NEC wametutaarifu
kwa barua juu ya hilo na sisi tumeshatekeleza wajibu wetu wa kupeleka majina
manane, na wao wameshatekeleza na kuteua na nakala wametupa,” alisema Mneke.
Alisema kwa upande wa madiwani hao wawili,
tayari chama kimeshaandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri za
Manispaa za Ubungo na Temeke jijini Dar es Salaam, kuwataarifu uwepo wa nafasi
hizo na wanachosubiri ni majibu ya barua hizo.
“Pia kwa nafasi za madiwani, tumeshawaandikia
wenyeviti husika barua kuwajulisha uwepo wa nafasi za madiwani tunachosubiri ni
majibu yao na ndipo hatua nyingine zifuate,” alisema Mneke.
Aidha, aliwatahadharisha wanachama wa chama
hicho kuwa bado mchakato wa kuwafukuza wasaliti ndani ya chama, unaendelea na
iwapo wabunge hata wa majimbo watabainika kuhusika watachukuliwa hatua za
kinidhamu.
Wakizungumzia kuvuliwa kwao uanachama, Kiongozi
wa wabunge wa CUF Bungeni ambaye naye amevuliwa uanachama, Riziki Ngwali
alisema hadi sasa hawajapokea barua rasmi ya kuvuliwa uanachama wao.
Alisisitiza kwamba walichaguliwa kwa barua na
lazima watenguliwe kwa barua. “Hatujapokea barua hadi sasa, lakini pamoja na
hilo, sisi hatukubali uamuzi huo kwa sababu haujatolewa na mamlaka sahihi,
tumeamua kwenda mahakamani kutafuta haki yetu,” alisema Ngwali.
Julai 25, mwaka huu Ofisi ya Spika wa Bunge,
ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema imepokea barua kutoka kwa
Mwenyekiti wa Taifa ya CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ikimuarifu kuhusu uamuzi wa
Baraza Kuu la Chama hicho, kuwafukuza wabunge wanane na madiwani wawili
uanachama wa chama hicho kwa makosa kadhaa ya kinidhamu.
Wabunge waliofukuzwa uanachama na kuvuliwa
ubunge wa viti maalumu ni pamoja na Serevini Silvanus Mwijage, Saumu Heri
Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa,
Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Alli Mohamed.
Chanzo: Habari leo.
No comments:
Post a Comment