Baraza Kuu la Waislam Tanzania(Bakwata) limeelezea sababu za mufti mkuu Abubakary Zuberi kudaiwa kutaka kuondolewa katika madaraka yake hayo.
Pia limesema tume ya kufuatilia mali za waislam tayari imeshatoa ripoti tatu na bado inaendelea kubaini mali za waislam zilizopotea kinyemela.
Akizungumza jijini Dar es salaam leo mwenyekiti wa halmashuri kuu baraza kuu Bakwata na msemaji wa bakwata, sheikh Khamis Mataka amesema pamoja na mambo mengine mabadiliko ya kimfumo na kiutendaji ni miongoni mwa sababu za kuwapo kwa taarifa ya kutaka kumuondoa mufti Zuberi.
Amesema pia kumekuwa na madai ya wafanyakazi wa bakwata makao makuu walia njaa na mgogoro wa walimu wa sekondari Bondeni ya mkoani Arusha.
"Hakuna njama zozote za kumuondoa Mufti madarakani, hakuna ubadhilifu wowote unaotuhumiwa nao na kwa hakika ni kuwa hakuna kipindi chochote ambacho baraza limeimarika na kufanya mambo yake kwa mujibu wa katiba kuliko kipindi hiki, "amesema.
Amesema baraza hilo ni imara na kwamba linaendelea kuzipatia majibu ya kimfumo changamoto ilizozikabili kwa muda mrefu.
Amesema baraza hilo litasimamia falsafa ya Mufti Zuberi ya 'Jitambue, Badilika, Acha Mazoea' katika kusimamia mabadiliko ya kimfumo na kiuendeshaji ndani ya baraza hilo.
"Wale wote watakaobainika kukwaza juhudi hizi kwa kuzusha fitna na kula njama ya kulivuruga baraza, Bakwata itawachukulia hatua stahiki bila ya kuangalia sura wala nafasi zao katika baraza au katika jamii, "amesema.
Akizungumzia mafao ya wafanyakazi wa baraza hilo, Sheikh Mataka amekiri kudaiwa sh milioni 176.
Katika hatua nyingine, sheikh Mataka amesema walimu wa shule ya sekondari Bondeni mkoani Arusha wameshalipwa mishahara yao waliyokuwa wakidai ya miezi miwili.
"Bakwata inawaomba waislamu kuunga mkono mabadiliko ya kimfumo na kiutawala yanayoendelea ndani ya Bakwata kupitia mamlaka mbalimbali za kikatiba zilizopo, "amesema.
Amesema kutimia kwa mabadiliko hayo kutaliwezesha baraza hilo kujitegemea, kuimarika kiutendaji na kuwahudumia waislamu na taifa kwa namna inayostahili.
Na Salha Mohamed, Dar es salaam
No comments:
Post a Comment