Na mwandishi wetu
WAZIRI mkuu, Kassim Majaliwa amekipiga marufuku Chuo Kikuu Ardhi kukodi kampuni ya kufanya kazi za ukadiriaji majenzi kwa niaba ya chuo hicho.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akirudisha mkasi baada ya kukata utepe kuashiria ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya miaka 10 chuo kikuu cha Ardhi.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati wa ugunguzi wa kongamano la maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa chuo kikuu cha Ardhi.
Amesema kitendo hicho kinaharibu kazi na sifa ya chuo hicho kwa kuwa baadhi ya kampuni wanazozipa kazi hazikidhi vigezo.
“Kama kuna umuhimu wa kufanya kazi na kampuni ni bora muanzishe kampuni ya kwenu itakayofanya kazi vizuri ili kujiepusha na matatizo.” amesema.
Pia Waziri Mkuu amekiagiza chuo hicho kufanya tafiti zenye kuleta majibu ya maswali na changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa na Dunia.
Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi holela,
uharibifu wa mazingira na majanga ya asili kama mafuriko.
Amesema Serikali inaamini kuwa matokeo ya kazi zinazofanywa na chuo hicho zikiwemo tafiti ni chachu ya maendeleo ya taasisi za elimu ya juu.
Waziri Majaliwa pia amekitaka chuo hicho kufanya tafiti, usanifu majengo na ujenzi kwa gharama nafuu ili kuisaidia jamii.
No comments:
Post a Comment