Habari za wakati huu msomaji wa wingu la habari, bila shaka nina
imani enaendelea vizuri na kama kuna matatizo
basi mimi naendelea kukuombea ili uweze kukabiliana na changamoto ambazo kwa namna
moja hama nyingine zinakufanya kutokamilisha mipango yako kwa wakati.
Kama kawaida kila siku ya Juma pili uwa nakuletea Makala ya
uchumi lengo ikiwa ni kukumbushana kipi ambacho unatakiwa kufanya katika sekta
ya uchumi na kutimiza malengo yako kwa
wakati, kwani asilimia kubwa ya watu ususani vijana wanapopata fedha
wanashindwa kufanya mambo ya kimaendeleo na kujikuta wanatumia katika matumizi
ambayo sio ya lazima kwao.
Katika maisha ya kila siku tunayoishi nidhamu ni kitu bora , na
leo nitazungumzia nidhamu ya matumizi ya fedha na kukufanya kufanikiwa katika
maisha yako katika maswala ya kiuchumi,
nidhamu katika matumizi ya fedha ndiyo nguzo pekee inayoweza kumfikisha mtu
kwenye kiwango cha mafanikio anachokitaka, hata kama kipato cha mtu huyo ni
kidogo kiasi gani, hivyo kufikia malengo aliyojiwekea.
Bila shaka uliwahi kuwaona watu
wawili wanaofanya kazi katika kampuni moja, wakifanya kazi moja na kulipwa
mshahara sawa, lakini wakawa na mafanikio tofauti, kwa mmoja wao kuweza kujenga
nyumba yake ya kisasa ya kuishi yeye na familia yake huku mwenzake akiendelea
kupanga chumba mjini, huku wote wakiwa na ukubwa wa familia ulio sawa.
Na wakati mwengine umewahi kuwaona watu wawili wanaofanya kazi
katika kampuni moja, wakifanya kazi moja na kulipwa mshahara sawa, lakini mmoja
wao ana miradi yake nje ya kazi au kutafuta vyanzo vingine vya kumwingizia
kipato nje ya muda wa kazi, huku mwingine akisubiri tu mshahara wake wa mwisho
wa mwezi kama kwamba kwake bila mshahara hakuna maisha.
Kitu gani kinawatofautisha
kimaendeleo watu hao wawili wakati wote wanalipwa stahiki zinazofanana, lakini Kubwa linalowatofautisha hapa ni nidhamu ya
matumizi ya fedha katika mpangilio wa
matumizi yao kutokana na mshahara wao wa mwezi.
Msomaji wangu leo nakuletea nguzo nne za kuyafikia malengo ya mafanikio kiuchumi
katika maisha. Nguzo hizo nne ni nidhamu
katika matumizi ya fedha, kufanya kazi kwa bidii na kujituma, kutoa huduma bora
kwa wateja na upekee na ubunifu unaweza kuhimili ushindani katika soko.
Hivyo leo tutazungumzia nguzo moja ya kwanza inayohusu nidhamu katika mpangilio
na matumizi ya fedha.Kwani kuna
wajasiriamali wengi tu wanaofanya biashara ya kuuza mchicha, sukuma wiki, mnafu
,matunda na kadhalika.
Aidha, kuna wafanyakazi walioajiriwa
katika taasisi kubwa kama vile serikalini, mashirika ya umma na makampuni
binafsi makubwa.
Lakini, katika makundi haya mawili,
kundi la wajasiriamali waunza mboga mboga na kundi la wafanyakazi walioajiriwa
katika taasisi kubwa, unaweza kukuta huyu anayeuza mboga akiwa anamiliki nyumba
nzuri, anasomesha watoto wake katika shule nzuri, na halafu huyu aliyeajiriwa
na kupata mshahara kwa mwezi akawa hana hata kibanda, huku akiwa haishiwi na
madeni yanayotokana na mikopo.
Nini kinatokea kwa kwa wawili hao wakawa
na tofauti hiyo ya maisha, Jibu ni moja tu. Mmoja wao ana nidhamu ya fedha,
mwingine hana nidhamu hiyo wala hana malengo yoyote kuhusu maisha yake.
Bila nidhamu ya fedha ni vigumu
kufanikiwa kimaisha. Watu wengi wameshindwa kusonga mbele kiuchumi, na badala
yake kujikuta wakidumaa kiuchumi kwa sababu ya kukosa nidhamu hiyo. Watu wa
aina hii, maisha yao yote, miaka nenda rudi, yanakuwa ni yale yale, hayabadiliki
kwa kuwa na hali nzuri.
Siri ya mafanikio ipo katika kila
jinsi unavyoipangilia na kutumia kila senti moja inayopita mikononi mwako. Ni
muhimu kwa yeyote mwenye nia ya kufikia malengo fulani ya kiuchumi,
kujitathimini ni kwa vipi anatumia kila senti inayopita mkononi mwake. Je,
sehemu ya kila senti hiyo inayopatikana, inawekwa akiba ili iongezeke ama
inatumika kuzalisha senti nyingine au anaitumia mara moja na kusahau?
Kutokuwa na nidhamu ya fedha
kumewasababishia baadhi ya watu kufilisika na kugeuka kuwa ombaomba, pamoja na
kwamba kabla ya kufilisika walikuwa na fursa hata ya kwenda kukopa fedha kwenye
taasisi za fedha.
Katika dunia ya sasa, bado kuna
baadhi ya watu wamegeuka kuwa watumwa wa maisha kutokana na tabia yao ya kutaka
kujionyesha kwa watu kwamba wanazo fedha za kutumia, hata kama fedha hizo
wanazipata kwa shinda.
Kwa hakika kabisa, watu wa aina hii,
hufika mahali wakayajutia maisha yao pindi kipato hicho wanachokichezea leo
kutokana na kutokuwa na nidhamu ya fedha kuyeyuka, kwa sababu tu ya kuhendekeza
starehe.
Wanasahau kwamba katika dunia ya
sasa, heshima ya mtu inakuwepo kutokana na mafanikio aliyonayo mtu kiuchumi,
hasa ushiriki wake kikamilifu katika shughuli za kijamii zinazohusiana na
maendeleo yao kwa ujumla.
Hata hivyo, msingi mkuu wa nidhamu ya
fedha ni familia. Wazazi hawana budi kuwa mfano bora wa nidhamu katika matumizi
ya fedha kwa watoto wao ili nao, kwa kuiga mfano wa maisha ya wazazi wao,
waweze kufanikiwa kiuchumi.
Mimi
ninaamini yeyote anayeamua kuchukua hatua sasa, kwa kuthubutu kubadilisha tabia
yake juu ya nidhamu katika matumizi ya fedha zake, mafanikio katika maisha
yanapatikana kwa njia ya mteremko tu. Fanya uamuzi sasa ili uwe kati ya
miongoni mwa watu waliofanikiwa kiuchumi.
Mwiki ijayo nitazungumzia nguzo ya
pili ambayo ni Kufanya kazi kwa bidii na kujituma.

No comments:
Post a Comment